Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeeleza kusikitishwa kwake na ajali ya gari moshi iliyotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imesema kuwa, serikali na wananchi wa Iran wanatoa mkono wa pole kwa serikali, wananchi na waathirika wa ajali hiyo iliyotokea katika jimbo la Katanga. Dikanga Kazadi Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kongo alitangaza jana kwamba, kwa akali watu 56 walipoteza maisha na wengine 69 kujeruhiwa kwenye ajali hiyo iliyosababishwa na gari moshi kuacha njia ya reli katika jimbo la Katanga. Waziri Kazadi ameongeza kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo kutokana na baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo kuwa mahututi. Ajali hiyo imetokea baada ya gari moshi la mizigo kubeba abiria karibu na mji wenye utajiri wa madini wa Likasi, ambao uko kati ya miji ya Lubumbashi na Kolwezi. Taarifa zinasema kuwa, ajali nyingi za reli nchini Kongo zinatokana na uchakavu wa reli. Inafaa kuashiria hapa kuwa, mwezi Disemba mwaka 2012, watu wasiopungua 37 walipoteza maisha baada ya kutokea ajali ya gari moshi katika mji wa Lubumbashi nchini humo.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
0 comments:
Chapisha Maoni