Matumizi ya kijeshi duniani yamepungua katika mwaka wa 2013 kutokana na kupungua kwa matumizi nchini Marekani na katika mataifa mengine ya magharibi, lakini matumizi katika mataifa yanayoinukia kiuchumi yameongezeka.
Shirika la kimataifa la utafiti wa amani la mjini Stockholm SIPRI, limesema kuwa punguzo la asilimia 1.9 katika matumizi ya kijeshi duniani limefuatia punguzo lingine la asilimia 0.4 mwaka 2012.
Lakini ripoti hiyo ya SIPRI imebainisha kuwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka kumi, Urusi ilitumia kiasi kikubwa zaidi cha jumla ya uchumi wake mwaka 2013 katika kuwekeza kwenye ununuzi wa zana za kijeshi kuliko Marekani, wakati nchi hiyo ikijaribu kuimarisha uwezo wake wa kijeshi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matumizi ya kijeshi ya Urusi yaliongezeka kwa asilimia 4.8 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 87.8, hii ikiwakilisha asilimia 4.1 ya pato lake la jumla la ndani.
Mpango wenye makuu
Mkurugenzi wa programu wa SIPRI Sam Perlo-Freeman, alisema ongezeko hilo katika matumizi ya Urusi linaendana na mpango wa kuimarisha nguvu za kijeshi za taifa hilo wa mwaka 2011 hadi 2020, ambao unalenga kutumia jumla ya dola milion 700 kuwekeza katika zana teknolojia na sekta nzima.
Lakini aliongeza kuwa changamoto za kiuchumi zinaweza kuizuwia Urusi kuongeza matumizi yake ya kijeshi haraka kama ilivyotarajiwa, licha ya mgogoro unaoendelea nchini Ukraine. Hata wachambuzi wa kiuchumi wanaamini mpango umejengwa katika misingi ya matarajio yaliyopitiliza.
Marekani ilikataa matumizi yake kwa asilimia 7.8 mwaka 2013, lakini imeendelea kuwa muwekezaji mkubwa zaidi katika sekta ya kijeshi duniani, kwa kutumia dola bilioni 640 au asilimia 3.8 ya pato la jumla la ndani.
Kupungua huku kumetokana hasa na kumalizika kwa vita vya Iraq, na kuanza kuondolewa kwa vikosi vya kimataifa nchini Afghanistan na athari za makato ya moja kwa moja ya bajeti yalioidhinishwa na bunge la Marekani.
Angola, Algeria zaongoza AfrikaUkubwa wa bajeti ya Marekani ulikuwa sawa na jumla ya mataifa mengine tisa yaliyo na matumizi ya juu duniani, ambayo pamoja na Urusi yanazihusisha China ambayo ilishika nafasi y apili kwa kutumia dola bilioni 188, Saudi Arabia iliyotumia dola bilioni 67, huku Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Japan, India na Korea Kusini zikikamilisha orodha ya watumiaji 10 wa juu.
SIPRI imesema kumekuwa na mwelekeo mpya katika miaka ya hivi karibuni, ambapo matumizi ya kijeshi yanapungua katika Amerika ya Kaskazini, Ulaya na Oceania wakati katika maeneo mengine matumizi haya yanaongezeka.
Barani Afrika Angola na Algeria zilielezwa kuwa na matumizi makubwa ya kijeshi, zikitumia fedha za mauzo ya mafuta na gesi. Mataifa hayo mawili ni miongoni mwa mataifa mengine 23 yalioongeza matumizi yake mara mbili tangu mwaka 2004.
Mengine ni pamoja na Afghanistan, Argentina, Armenia, Azerbaijan, China, Ghana, Paraguay, Urusi na Saudi Arabia. Taarifa za SIPRI zinaonyesha kuwa dunia ilitumia jumla ya dola trilioni 1.75 katika bajeti za kijeshi mwaka 2013.
0 comments:
Chapisha Maoni