Mwendesha mashtaka mmoja nchini Ufaransa anasema mshukiwa mkuu wa mashambulio ya Paris mwaka jana Salah Abdeslam amekiri kwamba alitaka kujilipua, lakini akabadilisha nia yake.
Abdeslam alikamatwa Ijumaa mjini Brussels, Ubelgiji na amefunguliwa mashtaka ya ugaidi.
Mwendesha mashtaka wa Paris Francois Molins ameambia kikao cha wanahabari: "Salah Abdeslam leo akihojiwa na wachunguzi (wa Ubelgiji) amekiri kwamba, na nanukuu, ‘alitaka kujilipua akiwa Stade de France lakini akabadili mpango wake’.”
Madai ya Abdeslam yanafaa kuchukuliwa kwa tahadhari hata hivyo, ameongeza.
Abdeslam, 26, ambaye ni raia wa Ufaransa aliyezaliwa Ubelgiji, anazuiliwa na polisi baada ya kukamatwa Ijumaa mjini Brussels baada ya kuwa mtoro kwa miezi minne.
Wachunguzi wanatumai mshukiwa huyo, aliyepigwa risasi mguuni wakati wa kukamatwa, atafichua habari zaidi kuhusu mtandao wa kundi linalojiita Islamic State (IS) uliopanga mashambulio ya Paris, na wafadhili.
Wanaamini alisaidia katika mipango, ikiwemo kukodisha nyumba na kuwasafirisha walipuaji wa kujitoa mhanga walioshambulia Stade de France.
Wakili wa mshukiwa huyo anasema atapinga jaribio la kumpeleka Ufaransa akajibu mashtaka zaidi lakini anaendelea kushirikiana na polisi.
Mashambulio ya Paris yaliyotekelezwa 13 Novemba mwaka jana yaliua watu 130 na kujeruhi wengi.
0 comments:
Chapisha Maoni