.

.

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AMEFUATILIA KUAGWA KWA MIILI YA WATU WALIOPOTEZA MAISHA KATIKA AJALI YA NDEGE.

NA JACKLINE LENDAVA.



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameacha shughuli zingine anafuatilia tukio la kuaga miili ya watu waliofariki katika ajali ya ndege kwa njia ya mtandao na ametoa pole kwa wanabukoba, wanakagera na Watanzania wote kwa msiba huu.

Ameyasema hayo alipokuwa akiongoza mamia ya watanzania katika uwanja wa ndege Kaitaba mkoani Kagera wakati wa kuaga miili ya watu 19 waliopoteza maisha katika ajali ya ndege iliyotokea Novemba 06, 2022.

Waziri Mkuu amesema kuwa baada ya ajali hii, hatua zilizochukuliwa ni kuratibu shughuli za kuondoa majeruhi, kushirikiana na wananchi kuwaokoa ndugu na kuwakimbiza hospitali kwa ajili ya matibabu, kusimamia na kutoa huduma za haraka za matibabu kwa majeruhi.

"Serikali imekamilisha taratibu za kutambua miili ya baadhi ya ndugu zetu waliofariki katika ajali hii ya ndege, kuwasitiri waliofariki, kutoa taarifa kwa umma na Serikali kuleta wataalam wa uchunguzi wa awali wa chanzo cha ajali."

"Nawasihi wananchi kuwa watulivu mpaka hapo timu ya wataalam itakapokamilisha zoezi na kutoa taarifa kwa umma baada ya uchunguzi kukamilika." Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. 



Mhe. Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza kijana aliyeiona ndege ikitua kwenye maji na kwa ujasiri wake akaamua kwenda kufungua mlango akabidhiwe kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ili apatiwe nafasi katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

"Naendelea kutoa pongezi na shukurani za dhati kwa wote walioshiriki katika zoezi la uokoaji tangu jana ajali hii ilipotokea mpaka wakati huu tunavyowaaga wapendwa wetu."

"Nawapongeza pia Wavuvi kwa kutoa msaada wa uokozi, kwa mchango wenu mliouonesha namuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Maafa kufika kuonana na kundi la wavuvi ili kuona namna wanavyoweza kuwaendeleza kwa kuwapatia mafunzo ya maafa." Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. 

Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuwa mazishi ya wahanga wote yagaharamiwe na Serikali, hivyo Wakuu wa Mikoa katika maeneo husika wasimamie kikamilifu mazishi ya waliotangulia mbele za haki. 

"Kamati za usimamizi wa maafa katika ngazi ya Mikoa  na Halmashauri zitaendelea kuimarishwa ili ziweze kuchukua hatua za haraka pale maafa yanapotokea katika maeneo yao na serikali itaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha usafiri wa anga unakuwa salama na unazingatia viwango vinavyohitajika kitaifa na kimataifa, ninawatoa hofu Watanzania kuwa tuendelee kutumia usafiri wa anga kwa kuwa Mamlaka husika zipo na zinasimamia na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha uwepo wa usalama wa anga kwa ajili ya safari za ndani ya nchi." Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. 

Waziri wa ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema kwamba wana familia, wananchi wa Mkoa wa Kagera, Watanzania wote na Sekta ya Usafiri wa Anga kwa ujumla wamekuwa kwenye majonzi kwa kuondokewa na ndugu zetu 19.

Pia taarifa ya awali ya hali ya hewa katika uwanja wa Ndege wa Bukoba jana ilionyesha mnamo saa mbili asubuhi hali ya hewa ilikuwa shwari sana.

"Hali ilibadilika ghafla ilipofika saa 2:20 asubuhi wakati Rubani yupo katika hatua ya mwisho kutua katika uwanja huo. Kulikuwa na mvua, zilizoambatana na radi zenye upepo mkali wenye mgandamizo wa kwenda chini."

Ameongeza kuwa "timu ya wataalamu ipo kwenye eneo la ajali tokea jana na uchunguzi wa ajali ya ndege hiyo unaendelea. Ajali zote za ndege zina taratibu zake na tunaendelea kuzifuata hatua kwa hatua kwenye uchunguzi wa ajali ya ndege hii." Waziri Makame. 

Waziri Makame amesema kuwa kwa sasa ndege ndogo zina uwezo wa kutua na kuruka katika uwanja huo, mpaka itakapofika jioni ya leo, ndege ya Air Tanzania Bombardier q400 inaweza kutua na kuruka kwenye uwanja huu wa Bukoba.

"Naomba niwahakikishie Watanzania wenzangu, usafiri wa anga nchini upo salama sana, ndio usafiri salama sana duniani, tuendelee kuutumia usafiri huu wa anga, iliyotokea jana ni bahati mbaya sana, na tunaamini haitakuja kutokea tena siku zijazo" Waziri Makame. 

Pia waziri wa ulinzi wa Jeshi la Kujenga Taifa mhe. Innocent Bashungwa ameatoa pole kwa msiba huo mkubwa uliolipata Taifa na kusema ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu hivyo hatuna budi kumshukuru Mungu na kuwaombea Marehemu wote wapumzike kwa amani na majeruhi afya zao ziimarike.

"Katika tukio lolote tunapata fursa ya kujifunza, katika tukio hili la ajali tumepokea maoni kutoka kwa wananchi ya namna tunavyohitaji kujipanga vyema zaidi katika kuboresha mfumo wa uokoaji, Serikali yetu ni sikivu imeyachukua maoni haya na itayafanyia kazi."

Ameendelea kusema kuwa "Tumeona sekta binafsi ilivyoshiriki katika suala la uokoaji kwenye ajali hii, hivyo kupitia Kurugenzi ya Maafa na Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama tutajipanga kuhakikisha tunashirikiana na sekta binafsi." Waziri Bashungwa. 



Naye waziri wa mambo ya ndani ya Nchi Mhe. Hamad Masauni amesema serikali inaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha inaviwezesha vyombo vyetu vya usalama ili viweze kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na majanga mbalimbali.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kagera mhe. Albert Chalamila amesema kuwa ajali hiyo imetokea Bukoba mkoani Kagera na imeleta madhara kwa wananchi, ndege ilikuwa na watu 43 ambapo wasafiri ni 39, wahudumu wa ndege wawili, Rubani mmoja na Msaidizi wa Rubani mmoja na watu waliofariki katika ajali hiyo ya ndege ni 19 na waliookolewa ni 24.

"Natoa rai kwa wananchi kuwa ajali kama hizi zikitokea tusiungane na wale wachache wanaoeneza habari za uongo, tusilitumie tukio hili kisiasa maana tayari tumeshapoteza wenzetu."

"Namshukuru  Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa wema wake mkubwa kwani amekuwa mfariji mkubwa tangu tukio hili lilipotokea, nawashukuru pia na viongozi wengine wa Serikali kwa kuwa nasi bega kwa bega na kwa kutufariji." Amesema Chalamila. 

Pia amewashukuru wananchi pamoja na wavuvi waliokuwa kandokando ya ziwa Victoria, mmliki wa gereji na magari makubwa ambaye amesaidia bila kulipwa chochote, Chuo cha VETA - Kagera kwa kutoa kamba ya kuvutia ndege, Jeshi la Zimamoto na Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wenzetu wa GGM kushirikiana nasi kuitoa ndege kwenye maji. 



Aidha amewashukuru Songoro Marine, TPA, TANESCO, TAA, Shirika la Ndege la Precision, viongozi wa dini, madaktari, Shirika la Msalaba Mwekundu pamoja na Kiwanda cha Sukari cha Kagera kwa kuleta mitambo yao pamoja na kuchangia rambirambi ya Shilingi milioni moja kwa kila mfiwa.

Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma nao wote wametuma salamu za pole na wanaungana nasi katika wakati huu mgumu.

Share on Google Plus

About Dira Ya Maisha

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Chapisha Maoni