Mwandishi Wetu
Taasisi ya Waandishi wa Habari ya Kusaidia Jamii za Pembezoni (MAIPAC) imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari nchini kuhusu uandishi wakati wa migogoro unaozingatia usalama binafsi na kulinda amani.
Mafunzo hayo yamewashirikisha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Mara, Manyara, Mbeya na Arusha, na yalidhaminiwa na Shirika la Wanahabari la Press Unlimited.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma, aliwataka wanahabari wanaokwenda kuripoti migogoro kuzingatia tahadhari za kiusalama na kuepuka upendeleo wa upande wowote.
Juma alisema kuwa habari za upande mmoja zisizozingatia maadili ya taaluma na maslahi mapana ya umma zimekuwa zikichochea migogoro katika jamii.
Aidha, aliwataka wanahabari kuzingatia usalama wao wakati wote wa kazi zao, kufanya upembuzi yakinifu wa kina kabla na baada ya kuchapisha habari, na kutathmini athari za taarifa wanazozitoa.
“Tujiulize habari ina madhara gani au ina faida gani kwa jamii. Tusiwe na upande katika habari na tuzingatie tahadhari za kiusalama tunapotumia vyombo vya kidijitali pamoja na kujilinda binafsi,” alisema Juma.
Kwa upande wake, Wakili wa kujitegemea, John Sendodo, akitoa mafunzo kuhusu sheria mbalimbali za masuala ya habari, aliwataka wanahabari kuzifahamu na kuzizingatia sheria hizo hata kama zina mapungufu.
“Kuna sheria kadhaa ambazo lazima mzijue, ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni na nyinginezo. Ni muhimu kuzisoma na kuzifahamu,” alisema Sendodo.
Wakili Sendodo, ambaye anafanya kazi na shirika la kimataifa la Protection Africa, alifafanua vifungu vya sheria hizo pamoja na mikataba kadhaa ya kimataifa inayohusu wanahabari, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi bila kuvunja sheria huku wakitekeleza wajibu wao kwa weledi.
Naye mmiliki wa Chuo cha Waandishi wa Habari cha Fanikiwa kilichopo Arusha, Joseph Mayagilla, aliwataka wanahabari kuzingatia maadili ya uandishi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mayagilla alisema habari za upande mmoja zimeleta madhara katika jamii na kubainisha kuwa kumekuwepo na ongezeko la uandishi usiozingatia maadili ya taaluma.
Aliongeza kuwa ili kuboresha ubora wa habari, ni muhimu kurejesha madawati maalum katika vyombo vya habari, yakiwemo madawati ya uchunguzi, amani na maendeleo, uchumi na mengineyo, yatakayoongozwa na waandishi wabobezi katika maeneo husika.
Kwa upande wake, mtaalamu wa saikolojia, Ester Cornelio, aliwataka wanahabari wanaokabiliwa na msongo wa mawazo kutojifungia bali kutafuta msaada wa kitaalamu.
Alisema kunywa pombe kupita kiasi au kuvuta sigara hakuondoi msongo wa mawazo (trauma), bali tiba sahihi ni kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya ya akili.
Cornelio alibainisha kuwa wanaume mara nyingi huathirika zaidi na msongo wa mawazo au sonona kwa sababu hawazungumzi na kutoa hisia zao kwa urahisi, tofauti na wanawake.
Wakichangia mada katika mafunzo hayo, Mwanahabari Tausi Mbowe, Meneja wa Dawati la Kidijitali Star TV, na Anthony Mayunga kutoka Serengeti Media, walisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya uandishi, kukabiliana na msongo wa mawazo na kuelewa changamoto za kisheria.
Tausi Mbowe alishauri kuimarishwa kwa mafunzo ya mara kwa mara kwa wanahabari, hasa kuhusu sheria na mbinu za kukabiliana na msongo wa mawazo.
Kwa upande wao, waandishi Elizabeth Nyivambe kutoka Mbeya, Muta Robert wa Geita na Zakaria Mtigandi wa Manyara, walisisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa mafunzo hususan katika matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na usalama wa wanahabari.
Mafunzo hayo yamelenga kuimarisha weledi, maadili na usalama wa wanahabari wanapotekeleza majukumu ya
o, hususan katika mazingira ya migogoro.






0 comments:
Chapisha Maoni