Na Jackline Lendava-Dodoma
Mamlaka ya hali ya hewa nchini imesema kuwa imepata mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa Rada, Vifaa na miundombinu ya hali ya hewa, kufungwa kwa Mitambo miwili (2) ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe inayohamishika na “measuring cylinders” zipatazo 100.
Mafanikio hayo yameelezwa na mkurugenzi wa huduma za utabiri (TMA) dkt. Hamza Kabelwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kueleza utekelezaji wa majukumu ya mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa Tanzania (TMA) na vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2022/23.
"Pia mafanikio mwngine ni pamoja na Seti tano (5) za vifaa vya kutambua matukio ya radi; Vifaa 15 vya kupima mgandamizo wa hali ya hewa; vifaa 25 vya kupima kiasi cha joto na unyevunyevu; mitambo minne (4) ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe; vifaa vya kupima mvua vinavyojiendesha vyenyewe, Mamlaka imepokea kompyuta maalum “Cluster Computer” ambayo ipo katika hatua ya ufungaji; Vilevile Mamlaka ilizinduwa mfumo mpya wa uangazi wa hali ya hewa ya anga ya juu katika kituo cha kupima hali ya hewa ya anga ya juu kilichopo JNIA."
Dkt Kabelwa ameongeza kuwa "Mamlaka imeendelea na utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu kupitia ofisi zake zilizopo kwenye Bandari za Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika. Katika mwaka 2021/22, idadi ya watumiaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya maji iliongezeka na kufikia 36,774 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19 ukilinganisha na watumiaji 32,736 waliohudumiwa katika mwaka 2020/21." Dkt. Hamza.
Pia dkt Kabelwa amesema kiwa katika kuangalia ustawi wa wafanyakazi, watumishi wa Mamlaka wameendelea kuboreshewa maslahi yao kupitia kupandishwa vyeo, kubadilishwa Kada na kuhuishwa kwa miundo ya kada kwa watumishi wa Mamlaka kufuatia Mabadiliko ya Miundo ya Maendeleo ya watumishi (Schemes of Services).
Aidha TMA imeendelea na utekelezaji wa mpango wa mafunzo kwa watumishi ambapo jumla ya wafanyakazi 50 walikuwa masomoni katika ngazi za (PhD, MSc, BSc and Diplomas) ndani na nje ya nchi, kati yao 3 PhD; 11 MSc.; 34 BSc.; 1 BA; na 2 ngazi ya shahada;
"Katika Utendaji wake Mamlaka ilitekeleza azma ya Serikali kwa kuhamishia Ofisi za Makao Makuu Dodoma ambapo kwa sasa Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania zipo katika Jengo la Chuo Kikuu cha Dodoma. Jitihada za kujenga jengo la Makao Makuu zinaendelea kufanyika ambapo tayari kiwanja kimeshapatikana."
"Kukamilika kwa ukarabati wa majengo ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa (National Meteorological Training Centre - NMTC) kilichopo mkoani Kigoma; Mamlaka imeendelea na ukarabati wa vituo vya hali ya hewa ambapo jumla ya vituo nane (8) vilivyopo katika mikoa ya Singida, Songwe, Dodoma, Tabora, Mpanda, Mahenge, Songea na Shinyanga vilikarabatiwa. " Dkt Hamza
Ameeleza mikakati waliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2022/23 kuwa ni kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa wananchi na wadau wengine juu ya umuhimu wa huduma za hali ya hewa,
kuimarisha uangazi wa hali ya hewa katika Bahari na Maziwa Makuu ili kuimarisha usalama wa abiria wa kwenye maji, shughuli za uvuvi pamoja na kusaidia shughuli mbalimbali zikiwemo upakuaji wa mizigo bandarini na uvunaji wa gesi asilia na
kufanya ufuatiliaji kwa wakandarasi wanaotengeneza Rada na vifaa vya hali ya hewa ili vikamilike na kuwasili nchini;
Kuongeza vyanzo vya mapato kwa lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa.
"Mikakati mingine ni kuhakikisha wadau wote wenye vifaa vya hali ya hewa nchini wanavifunga vifaa hivyo kwa kuzingatia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 na Kanuni zake, kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa, kuandaa miradi mbalimbali yenye lengo la kupata rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za hali ya hewa nchini." Dkt Hamza.
Dkt Kabelwe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa hapa nchini ikiwemo kutenga fedha katika bajeti ya Maendeleo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Sekta ya hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa vifaa hali ya hewa, upanuzi wa mtandao wa vituo vya hali ya hewa, ukarabati wa vituo vya hali ya hewa pamoja na ununuzi wa mitambo ya hali ya hewa ikiwemo Rada.
"Niendelee kuwaomba kwa kuwasisitiza kuboresha ushirikiano baina yetu hususan katika kuhabarisha umma kuhusu hali ya hewa ya kila siku, msimu na tahadhari, nazungumza hayo kwa kuwa Mamlaka imeandaa utaratibu mzuri wa kuwatumia taarifa hizo kila siku kupitia njia mbalimbali, mpaka hivi sasa vyombo vya habari tisini viko katika utaratibu huo."
"Natoa rai kwa wengine pia kuleta maombi ya kupata huduma hii muhimu kwa jamii na nchi kwa ujumla." Dkt Hamza.
0 comments:
Chapisha Maoni