Zaidi ya Waislamu 1,000 wametimuliwa katika mji wa Bossangoa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuelekea katika nchi jirani ya Chad huku kukiwa na hofu ya kuuawa kwa umati Waislamu mikononi mwa wanamgambo wa Kikristo.
Imearifiwa kuwa askari wa kikosi cha kulinda amani cha nchi za Afrika wamewasindikiza Waislamu kuondoka katika mji huo wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya kati mwa Afrika. Afisa mmoja wa polisi amenukuliwa na vyombo vya habari akisema. 'hakuna hata Mwislamu mmoja aliyesalia Bossangoa.'
Maelfu ya Waislamu wamezingirwa katika miji kadhaa huku magaidi wa Kikristo wajulikanao kama anti-Balaka wakiendelea kuwashambulia Waislamu wanaojaribu kuondoka katika nchi hiyo. Wiki iliyopita Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon amewataka wananchi, viongozi wa dini pamoja na pande hasimu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kujizuia ili kuilinda nchi yao dhidi ya kile alichokiita harufu ya mauaji ya kimbari.
Kuna askari karibu 2,000 wa Ufaransa na maelfu ya askari wengine wa kulinda amani kutoka nchi za Kiafrika huko Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini wameshindwa kuzuia mauaji ya Waislamu yanayofanywa na magaidi wa kundi la Kikristo la anti-Balaka
0 comments:
Chapisha Maoni