.

.

SULUHU YA KUANGAMIZA MDUDU MBUNG'O

 Na Deborah Lemmubi -Dodoma



Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania  TVLA kupitia kituo chake cha utafiti  VVBD waja na Suluhu kuangamiza mdudu Mbung'o aenezaye ugonjwa  wa Nagana kwa mifugo na Malale kwa binadamu kwa teknolojia ya vifukuzi na vivutizi.


Haya yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania TVLA Dr Stella Bitanyi, Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.



"Wakala kupitia kituo chake cha utafiti wa wadudu na magonjwa wayaenezayo cha VVBD Tanga hutoa huduma ya kuangamiza mbung'o katika maeneo yaliyo jirani na mbuga za wanyama. Mbung'o ni wadudu wanaoeneza ugonjwa wa Nagana kwa mifugo na Malale kwa binadamu. Kupitia tafiti za kuangamiza mbung'o, teknolojia mbalimbali zimeibuliwa ikiwa ni pamoja na matumizi ya mitego ya vitambaa inayonasa mbung'o pamoja na teknolojia ya vifukuzi na vivutizi"


"Vifukuzi ni kemikali zinazotoa harufu ya nguruwe pori ambaye hang'atwi na mbung'o hivyo vikifungwa kwenye shingo ya ng'ombe, mbung'o hawasogei. Vivuti ni aina ya kemikali ambayo huwekwa kwenye mitego na kuwavutia mbung'o na wakishaingia hawawezi kutoka. Kupitia teknolojia hizi kituo hiki cha utafiti kimefanikiwa kutokomeza mbung'o kutoka visiwa vya Zanzibar"


 Aidha Dk. Stella Bitanyi,amesema jumla ya sampuli 163,722 kutoka kwa wanyama mbalimbali zilipokelewa na kufanyiwa uchunguzi na utambuzi wa magonjwa.


Ambapo amesema kuwa njia za uchunguzi zilizotumika ni pamoja na kuchunguza vimelea vya magonjwa kwa kutumia hadubini kuchunguza viaashiria vya uwepo wa kinga dhidi ya kimelea kwenye damu kwa kutumia ELISA na kipimo cha juu kabisa cha uchunguzi wa aina ya kimelea kwa kutumia vinasaba yaani PCR.


“Katika kipindi cha miaka mitano kati ya 2017/2018 hadi Septemba 30, 2022 jumla ya sampuli 163,722 kutoka kwa wanyama mbalimbali zilipokelewa na kufanyiwa uchunguzi na utambuzi wa magonjwa.


“Magonjwa muhimu yaliyotambuliwa kwa wingi ni mdondo/kideri, ndigana baridi, ndigana kali, ndui kwa kuku, homa ya nguruwe, kimeta, ugonjwa wa kutupa mimba, homa ya mapafu ya ng’ombe, homaya mapafu ya mbuzi, kichaa cha mbwa, sotoka ya mbuzi na kondoo”


Kuhusu uzalishaji na usambazaji wa chanjo za mifugo, amesema Wakala inatekeleza jukumu hilo kupitia Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyoko Kibaha mkoani Pwani.


Amesema hivi sasa TVI, Kibaha inazalisha chanjo saba na uzalishaji kwa mwaka 2021/2022 ulifika dozi milioni 65.



“Kwakuwa chanjo haziwezi kuzalishwa na kusubiri wateja, kiwanda huzalisha kulingana na mahitaji ya soko. Uwezo kamili wa uzalishaji wa chanjo ni zaidi ya dozi milioni 100, kwa mwaka ambao hata hivyo bado haujafikiwa kutokana na uhitaji wa soko kuwa chini”


Hata hivyo ameeleza  kuwa ifikapo mwaka 2030, watu zaidi ya milioni 10, watakufa kila mwaka kutokana na matumizi holela ya dawa za mifugo ambayo yamekuwa yakisababishwa vimelea vya magonjwa kujenga usugu.


“Aidha matumizi ya dawa kiholela ya dawa hasa za aina ya antibaiotiki huweza pia kuwaathiri binadamu kutokana na kula mabaki ya dawa hizo kwenye vyakula vinavyotokana na wanyama”


Aidha, amesema hali hiyo ni tatizo kubwa linaloikabiri dunia kwa sasa na wafugaji wanapaswa kuzingatia ushauri unaotolewa ili kulidhibiti.


“Inakadiriwa kwamba kufikia 2030, watu zaidi ya milioni 10, watakufa kila mwaka kutokana na dawa kushidwa kuwatibu kwani vimelea vya magonjwa vitakuwa vimejenga usugu unaotokana na matumizi holela ya dawa kwa binadamu na mifugo”

Share on Google Plus

About Dira Ya Maisha

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Chapisha Maoni