eliaonesmo@gmail.com
Na Deborah Lemmubi-Dodoma
Taasisi ya Elimu ya Watu wazima Tanzania TEWW imefanikiwa kuwarejesha Shuleni wasichana 3,333 walioshindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito katika kipindi cha mwaka 2021/2022.
Ameyasema hayo mapema leo hii akiwa Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt.Michael Ng’umbi,wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Taasisi kwa mwaka 2021/2022 na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
”Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na mazigira magumu, kupata ujauzito au ndoa za utotoni kwa wenye umri kati ya miaka 13 hadi 21 ikiwa ni sawa na asilimi 111 ya lengo lililowekwa kupitia vituo 131 vinavyo hudumiwa na walimu 803"
Dr Ng'umbi amesema kuwa kazi zilizofanywa na taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, ni kuwa waliandaa na kuendesha mafunzo katika kampasi zake tatu Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza.Ambapo Programu tatu za mafunzo zilitolewa kwa njia ya ujifunzaji wa kawaida na kwa njia ya ujifunzaji huria na masafa.
“Programu hizo ni Elimu ya Watu Wazima na Mafunzo Endelezi, Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii, na Elimu Masafa kwa ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada”
Aidha amesema kuwa jumla ya wanafunzi 8,093 ambapo wanawake 4,644 na wanaume 3,449 walipata mafunzo hayo.
Pia, ameeleza kuwa taasisi hiyo ilifanya usajili wa wanafunzi wapya ambapo jumla ya wanafunzi 3,426 walisajiliwa katika programu tatu za TEWW kwa mwaka wa masomo 2021/22.
Aidha, jumla ya walimu na wasimamizi wa elimu ya watu wazima 2,355, walihitimu masomo yao katika mwaka 2021/22.
Vilevile, katika kipindi hicho taasisi hiyo iliandaa mtaala wa mafunzo ya walimu wa elimu ya watu wazima katika maeneo ya ufundi na teknolojia.
Aidha, mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza kutolewa kwa ngazi ya astashahada na stashahada katika mwaka wa masomo 2023/24 baada ya kuidhinishwa na NACTVET.
“Kwa mwaka 2022/2023, TEWW inatarajia kuendelea na utekelezaji wa jukumu hili ikiwa ni pamoja na kukamilisha mtaala wa mafunzo ya walimu wa elimu ya watu wazima katika maeneo ya ufundi na teknolojia na kupata idhini ya NACTVET”amesema
Hata hivyo amesema kuwa katika mwaka 2021/2022, TEWW ilipokea jumla ya maombi 62 kutoka kwa wadau wakiomba usajili wa kuendesha vituo vya shule huria za sekondari Tanzania bara.
Ambapo amesema kuwa ni waombaji 58 waliokidhi vigezo na kusajiliwa kwa mwaka 2021/22.
Dkt.Ng’umbi amemaliza kwa kutoa wito kwa wananchi kujiunga na programu za elimu ya watu wazima zinazotolewa na TEWW kwa sababu ni taasisi inayotoa elimu kwa nadharia na vitendo kwa kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuwa bora, mwenye kuweza kujiendeleza na kupambana na changamoto za maisha.
0 comments:
Chapisha Maoni