Na Jackline Lendava-Dodoma
Bodi ya Nyama Tanzania imesema ina jukumu na mkakati wa kuwahamasisha watanzania kula nyama, kwani ulaji wa nyama kwa kiasi kinachotakiwa ndio njia rahisi ya kuondokana na utapia mlo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Oktoba 28 Jijini Dodoma Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Dkt. Daniel Mushi wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022-2023, amesema kuwa kuna watu wamekuwa wakisema nyama ni mbaya lakini tatizo la ulaji wa nyama hutokana na kula nyama na kiasi cha nyama cha mtu anachokula na aina ya nyama anayokula.
"Niseme wazi hapa kuna mkanganyiko kidogo kuna watu wamesema nyama ni mbaya lakini suala la nyama kuwa mbaya au nzuri ni suala la kiasi cha nyama unachokula na aina gani ya nyama unakula." Dkt Mushi
Dkt.Mushi ameongeza kuwa ili mwili wa binadamu upate virutubisho vyote muhimu anatakiwa kwa wiki walau ale kilo moja ya nyama kwani virutubisho vinavyopatikana kwenye nyama nyekundu havipatikani kwenye mimea na kitaalamu mtu anapaswa kula nyama angalau kilo hamsini kwa mwaka.
Aidha amesema kuwa endapo mtu atakula nyama kwa kiwango kinachotakiwa atakuwa na afya kwani itasaidia kuimarisha kinga ya mwili ya kupambana na magonjwa nyemelezi na kuongeza nguvu ya kufanya kazi hivyo itasaidia kuongeza uzalishaji.
"Kama mnavyo fahamu nyama ndio njia rahisi ya kuondokana na utapia mlo, mtu anapowaambia watanzania wasile nyama nadhani haelewi vizuri hali ilivyo katika ulaji wa nyama na sisi kama Serikali tunao mpango wa kuhamasisha watanzania wale nyama lakini ulaji nyama uliosahihi." Dkt.Mushi
Sanjari na hilo amesema kuwa bodi itahakikisha inalinda afya ya mlaji kupitia udhibiti na ukaguzi sambamba na kuhamasisha uzajishaji bora wa nyama ili kupata masoko nje ya nchi.
Kwasasa mtanzania mmoja anakula nyama takribani kilo 15 kwa mwaka kuanzia Januari mpaka Disemba lakini ulaji sahihi ni kula nyama angalau kilo 50 kwa mwaka huku nje ya nchi wakila mpaka kilo 100 mtu mmoja kwa mwaka"
Sasa unapokula nyama kiasi kinachotakiwa kwanza unakuwa na afya unakuwa na nguvu ya kufanya kazi na uzalishaji unaongezeka lakini pia unakuwa na uwezo wa kinga ya mwili kuweza kujikinga na magonjwa kinga zinakuwa imara." Dkt.Mushi
Mwaka 2006 serikali ilitunga sheria ya tasnia ya nyama sura ya 421 yenye lengo la kuwezesha mabadiliko katika tasnia ya nyama, kuanzisha misingi thabiti ya usimamizi, kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa bora za nyama, kuendeleza ukuaji wa tasnia ya nyama na bodi ya nyama Tanzania ilianzishwa katika sheria hii ili kusimamia utekelezaji wa sheria husika.
0 comments:
Chapisha Maoni