Na Jackline Lendava-Dodoma.
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Muongozo wa matumizi wa matokeo ya sensa ya watu na makazi mara baada ya kutangaza matokeo ya Sensa ambayo imefanyika Agosti 23 mwaka huu.
Hayo yameelezwa na waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene na kusema kuwa muongozo huo ni muhimu kwani baada ya matokeo hayo kinachofuata ni matumizi.
Amesema kuwa takwimu zitakazopatikana zitasaidia katika shughuli mbalimbali za kupanga mipango zikiwemo taasisi za Umma, binafisi hata wafanyabiashara kwani serikali bila takwimu hizo haitapanga Mipango yake.
Waziri Simbachawene ameongeza kuwa huduma zote za kijamii kama hospitali, maji, umeme na masuala ya kilimo kuwepo kwa uhakika baada ya kuwa na takwimu.
"Kama ambavyo tumewatangazia hivi karibuni, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imo katika maandalizi ya Uzinduzi wa Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022 utakaofanyika katika uwanja wa Michezo wa Jamhuri hapa jijini Dodoma" Waziri Simbachawene.
Pia waziri Simbachawene ameongeza kuwa sherehe hiyo ya uzinduzi wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 zitahudhuriwa na viongozi wote wakuu wa Serikali pamoja na Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marais wastaafu wa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Marais hao wastaafu watatunukiwa tuzo maalum kwa kufanikisha Sensa katika vipindi vya uongozi.
Waalikwa wengine ni viongozi wa Serikali wakiwemo mawaziri na manaibu waziri, Makatibu wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Serikali zetu zote mbili, Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar, viongozi wa vyama vya Siasa na wawakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii.
Aidha, wageni wengine mashuhuri ni pamoja na Waheshimiwa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao humu nchini, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yakiwemo ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika; na Wadau wengine wa Maendeleo.
Katika Dodoma hii itakuwa historia kwa kuwa itakuwa mara ya kwanza kushuhudia tukio la uzinduzi wa Matokeo ya Sensa ambao ni fursa moja muhimu kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia uzinduzi huo ili kuonesha kuwa sio tu ni tukio la kihistoiria pia ni tukio linalotokea mara moja tu kila baada ya miaka kumi.
"Uzinduzi huu ni tukio moja muhimu katika historia ya maendeleo ya nchi hivyo ndio maana Serikali imeamua kuhakikisha kunakuwa na uwakilishi wa wananchi wa makundi yote ili waweze kushiriki katika tukio hili la kihistoria"
"Matokeo haya ni muhimu sana kwa makundi yote katika jamii, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji na hasa kwa Serikali yetu inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwani Serikali itaweza kupanga mipango yake kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kulingana na idadi, mahitaji na mazingira wanamoishi" Waziri Simbachawene
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar anaeshughulikia Sera Bunge,Uratibu, na Baraza la wawakilishi Hamza Hassan Juma amesema zoezi hilo lilienda vizuri kwa upande wa Zanzibar na taarifa zilizopatikana zitasaidia kujua idadi ya watu kujua kasi ya ukuaji kwa baadhi ya Mikoa .
"Takwimu hizi zitatusaidia sana na hasa katika masuala ya utafiti wenzetu wanaofanya tafiti zitasaidia kujua wanatafiti kuna watu wangapi" Hamza.
Tarehe 31 Oktoba, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika zoezi la kutangaza matokeo ya mwanzo ya sensa ya watu na makazi jijini Dodoma.
0 comments:
Chapisha Maoni