Na Jackline Lendava-Dodoma
Mkurugenzi wa Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Bi. Ziada Sellah ametoa wito kwa Wauguzi kwenda kuboresha utoaji huduma kwa wananchi pindi wataporejea katika maeneo yao, hasa katika kipindi ambacho Serikali inaelekea kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ili kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi.
Bi Ziada ameyasema hayo wakati akifunga Mkutano wa nne wa mafunzo ya kitaifa ya magonjwa yasiyoambukiza (NCD) kwa Wauguzi na Wakunga kutoka Mikoa ya Dodoma, Songwe, Lindi na Kigoma yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Amesema, Serikali inaelekea kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa wote itayotoa fursa kwa wananchi kwenda kupata huduma katika vituo vyovyote kuanzia ngazi ya Zahanati mpaka hospitali ya Taifa, hivyo kutoa wito kwa Wauguzi kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwemo suala ya matumizi ya lugha nzuri kila wakati.
“Niwaombe twende tukaboreshe huduma za Afya kwa wananchi kwasababu wengi wenye Magonjwa yasiyoambukiza wapo nyumbani na wengi wanashindwa kwenda kwenye matibabu kwasababu yakukosa kadi ya Bima, itavyokuja swala la Bima ya Afya kwa wote maana yake kila mtu atakuwa na uwezo kweda kupata huduma popote, kwahiyo niwasihi mkaboreshe huduma ili kuondoa matatizo yanayoweza kuzuilika." Bi Ziada
Ameongeza kuwa, Serikali imefanya jitihada kubwa katika kuboresha huduma nchini, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma, ununuzi wa dawa na vifaa tiba, kuajiri watumishi, hivyo kutoa wito kwa Watumishi kufanya kazi kwa weledi na kufuata misingi ya taratibu za mabaraza yao ya kitaaluma katika kuwaudumia wananchi.
Sambamba na hilo, Bi. Ziada ametoa wito kwa Wauguzi waliopata mafunzo hayo kupeleka ujuzi waliopata kwa Wataalamu wengine pindi watakaporudi katika maeneo yao ya kutolea huduma ili kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya magonjwa hayo.
Aidha, Bi Ziada amewataka Wauguzi kwenda kuanzisha kliniki za magonjwa yasiyoambukiza au kwenda kuziboresha ili wananchi wenye changamoto ya magonjwa hayo waanze kunufaika kwa kupata elimu na kupata matibabu dhidi ya magonjwa hayo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wakuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza Bi. Valeria Millinga amesema, moja kati ya mikakati iliyopo ni kuimarisha huduma za msingi kwa kuvijengea uwezo vituo vyote vya afya 600 kwa kuwapa mafunzo Watoa huduma angalau wanne katika kila kituo ili kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.
Naye mwakilishi wa Wauguzi waliopata mafunzo Bw. Richard Marwa amesema, mafunzo haya yamekuja wakati muafaka kwani kipaumbele cha Wizara ya Afya ni kutoa huduma bora kwa wananchi, huku kwa upande wa Wauguzi wameahidi kwenda kufanyia kazi yale yote waliyopata katika mafunzo hayo ikiwemo kuboresha huduma za magonjwa yote kwa wananchi.
0 comments:
Chapisha Maoni