Na Jackline Lendava Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Sheria ya Ustawi wa Jamii ikiundwa itarahisisha Uratibu wa utetezi wa haki za Makundi maalum.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa Chama cha Maafisa Ustawi wa Jamii(TASWO) jijini Dodoma Oktoba 26, 2022.
Amesema Maafisa Ustawi wa Jamii hawajapata Sheria ya kitaaluma inayowezesha kufanya kazi kama madaktari wa Jamii hivyo kutokuwa na Baraza la Ithibati kwa watoa Huduma za Ustawi wa Jamii.
"Natambua kiu yenu ya kutaka Serikali ifanikishe uundwaji wa sheria ya taaluma yenu, mtakumbuka suala la sheria ya Ustawi wa Jamii ni mojawapo ya mambo tuliyoyapa kipaumbele kwani ikiwepo itarahisisha Uratibu wa utetezi wa haki za Makundi Maalum" amesema Dkt. Gwajima.
Ameongeza kwamba, anatambua changamoto ya miundo inayochangia ugumu katika utekelezaji wa majukumu hasa ngazi ya mikoa na kwamba inafanyiwa kazi.
Mhe. Dkt. Gwajima amewahimiza Maafisa hao kushirikiana vema na wanajamii hasa wanaojitolea katika kutoa huduma za Ustawi wa Jamii katika kuhakikisha kazi yao inakuwa na ufanisi pamoja na uhaba uliopo, huku akiwapongeza wananchi waliojitolea kufanya kampeni maarufu ya SMAUJATA katika kutokomeza vitendo vya ukatili.
Amesema Kampeni hiyo imesaidia kuibua na kusaidia waathirika wa vitendo vya ukatili katika Mikoa yote kwa muda mfupi tangu ianzishwe mwezi Juni mwaka huu.
"Nina Imani mmeona nguvu ya Jamii ilivyo katika kuleta mabadiliko kupitia Kampeni ya SMAUJATA ambayo ni zao la Kampeni ya Wizara ya Twende Pamoja ukatili sasa basi" hivyo tunafanya tathmini na kuchukua maoni ya wadau wote Ili kuiboresha zaidi ameongeza Dkt. Gwajima.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi na Lishe Amina Mfaki amesema huduma mbalimbali zimetekelezwa kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii ikiwepo usuluhishi wa migogoro ya ndoa, kuhakikisha kesi za ukatili zinatolewa hukumu, kutambua watoto wanaoishi mazingira hatarishi, kuwatambua wazee, walemavu, waathirika wa madawa ya kulevya, na utoaji wa huduma za msaada wa Kisaikolojia.
Bi. Amina amesema mwezi Juni mwaka huu, Serikali imeajiri Maafisa Ustawi wa Jamii 819 ambapo wamefikia Maafisa 1017 kwani nguvu kazi inahitajika katika maeneo mbalimbai ya kutolea huduma.
Aidha, Bi. Amina amewataka Maafisa hao kufanya kazi kwa weledi, kuweka mipango kazi vema, kuandaa taarifa sahihi na kwa wakati kwa kutumia mifumo ya Ustawi wa Jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Ustawi wa Jamii nchini Dkt. Mariana Makuu ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na TASWO katika kuboresha mazingira ya utoaji wa Huduma mbalimbali.
"Ili kuwepo na Mazingira Bora na wataalamu kuendelea kufanya kazi ya kuimarisha Ustawi wa Jamii, tumeendelea kuona jitihada za makusudi za Serikali na Wadau katika kutatua changamoto mbalimbali" amesema Dkt. Mariana.
0 comments:
Chapisha Maoni