Na Jackline Lendava-Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan amewaasa viongozi wa dini nchini kuendelea kushikamana na serikali kudumisha uzalendo na amani ya nchi .
Ameyasema hayo Novemba 19.2022 Jijini Dodoma katika sherehe ya Jubilee ya miaka 50 ya Kanisa la Waadventista Wasabato ambapo amesema amani ndiyo msingi wa utulivu wa nchi.
"Nitumie fursa hii kulipongeza Kanisa la Waadventista Wasabato kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha amani na kuendelea kushirikiana na serikali kwa miradi mbalimbali ya huduma za kijamii ikiwemo sekta za afya, elimu na kusaidia wenye uhitaji." Rais Samia.
Aidha amekipongeza kikundi cha uimbaji cha watoto pamoja na Kwaya mbalimbali kwa kuimba nyimbo zenye uzalendo na upendo wa taifa la Tanzania.
"Kuhusu suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii niwaase viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na serikali kukemea vitendo viovu ikiwemo kushirikiana katika mapambano ya dawa za kulevya na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia." Rais Samia.
Aidha kwa upande wa suala la mabadiliko ya nchi ya ukosefu wa mvua katika baadhi ya maeneo amewaasa viongozi wa dini na washarika kwa ujumla kuliombea Taifa huku akitoa wito kwa viongozi wa dini kuwa mabalozi kuelimisha jamii kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira.
Hata hivyo Rais Samia amehitimisha kwa kusema kuwa ni muhimu kutegemea neema na Baraka za Mwenyezi Mungu kama isemavyo Zaburi 127:1.
Naye Mwenyekiti Kanisa la Waadventista Wasabato Union ya Kusini mwa Tanzania [STU] Mch.Dkt.Godwin Lekundayo amemhakikishia Rais Samia kuwa Kanisa litaendelea kushirikiana na serikali katika kuwajengea maadili vijana .
Mch.Lekundayo ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa serikali ya Tanzania kwa ajali ya ndege ya Precision Air iliyoua watu 19 hivi karibuni mkoani Kagera huku akisisitiza kuwa kanisa litaendelea kuiombea Tanzania kuepusha majanga.
Katibu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Kusini mwa Tanzania[STU] Mch.Jeremiah Izungo amesema wao kama kanisa wataendelea kushirikiana na serikali kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika sekta za elimu na afya.
Mch Izungo amesema kanisa linaendelea kusisitiza afya ya jamii ikiwemo kuzingatia kanuni bora za afya,lishe na kuchangia damu salama ambapo huwa kuna utaratibu wa kuchangia damu salama kila mwaka mwezi Machi.
Amesema changamoto zinazolikabili Kanisa ni pamoja na usaili wa nafasi za kazi serikalini siku ya Jumamosi ya ibaada ambapo hukosesha vijana nafasi za ajira serikalini pamoja na mitihani shuleni kufanyika siku ya Jumamosi ya ibaada.
Ameiomba serikali kuwapatia wataalam wabobezi katika hospitali za Kanisa huku akiweka msisitizo kuwa Kanisa linajitegemea haliko kwenye muunganiko wa wa Umoja wa Kikristo Tanzania [CCT].
0 comments:
Chapisha Maoni