Na Jackline Lendava-Dodoma.
Wakala wa maendeleo ya uongozi wa elimu kwa mwaka 2021/2022 umedahili Walimu 1,839 katika mafunzo ya Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu (DEMA) na Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule (DSQA) ili kuwapa ujuzi na maarifa walimu katika usimamizi, ufuatiliaji na tathimini katika elimu.
Hayo yameelezwa na mtendaji mkuu wa wakala wa maendeleo ya uongozi wa elimu (ADEM) dkt Sinton Mgullah wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya wakala huo na vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Amesema kuwa wakala umetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani, kwa Maafisa 3,860 (REOs, RAOs, DEOs, WEOs) ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji wenye kuleta tija katika elimu.
"Wakala umetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani kwa walimu 7,612 ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji katika shule wanazosimamia."
Ameongeza kuwa "wakala umeendesha mafunzo ya muda mfupi kwa Walimu Wakuu na Waratibu wa Taaluma 147 kutoka katika Shule za Msingi na Sekondari Zanzibar, chini ya mradi wa Mwanamke Initiative Foundation (MIF)." Dkt Mgullah.
Dkt Mgullah amesema wakala umefanya Tafiti sita na kuwasilishwa kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kubaini mapungufu na kuandaa mafunzo wezeshi kwa wahusika,
Sanjari na hayo wakala umeandaa Moduli 3 katika eneo la Uongozi na Usimamizi wa Shule ili kuendesha mafunzo ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa ujenzi wa umahiri kwa walimu wa Shule za Sekondari Zanzibar na umeandika vitabu vya kujenga umahiri katika utekelezaji wa Mtaala wa Sekondari ili kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza kwa ajili ya Shule za Zanzibar.
"Wakala unaendelea na ujenzi wa jengo la ghorofa moja katika kampasi ya Mbeya ili kuimarisha ufanisi katika shughuli za utoaji wa mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu. " Dkt Mgullah.
Dkt Mgullah ameeleza maleo ya wakala kwa mwaka 2022/23 kuwa ni kudahili Walimu 2,343 katika Kozi za CELMA, DEMA na DSQA, kuandaa Kiongozi cha Mwalimu Mkuu na kuandaa Mwongozo wa Utawala Bora kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.
"Tumejipanga kutoa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu wapatao 17,000, kutoa mafunzo ya utawala Bora kwa wasimamizi wa elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa."
"Kuhusu mafunzo kwa njia ya masafa, kwa sasa tuna mradi na wenzetu wa Chuo cha Mzumbe kwa ajili ya kuandaa Moduli za kuendeshea mafunzo ya masafa, tumeshafika mahali pazuri.
ADEM inatoa shukrani za pekee kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwapa fedha za ujenzi wa Kampasi ya Mbeya na kuendelea kutenga fedha za ukamilishaji wa ujenzi huo ambao kukamilika kwake kutaboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Kwa upande wake msemaji mkuu wa serikali ndg. Gerson Msigwa amesema serikali inaweka fedha nyingi kwenye sekta ya elimu nchi nzima ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23, sekta ya elimu pekee imetengewa Shilingi trilioni 5.8. Chuo hiki ni moja ya juhudi za Serikali za kusimamia ubora wa elimu.
"Fedha hizi ni nyingi ambazo zinahitaji usimamizi wa karibu, hivyo wale viongozi wa kwenye taasisi zinazosimamia elimu lazima wawe na ujuzi na mbinu nzuri za kusimamia maendeleo ya elimu ili tuweze kupata thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali."
"Natoa wito kwa waajiri kutosita kuwaruhusu viongozi wa taasisi za elimu kwenda kusoma ADEM." Ndg Msigwa.
0 comments:
Chapisha Maoni