.

.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaadhimisha miaka 50

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jana Jumamosi (26.04.2014) imeadhimisha miaka 50 tokea kuasisiwa kwake lakini sherehe hizo zimetiwa kiwingu na malumbano makali kuhusu mfumo wa muungano unavyopaswa kuwa.

Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete (Kushoto) na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein (Kulia).
Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete (Kushoto) na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein (Kulia).
Tanzania imezaliwa mwaka 1964 baada ya kuungana kwa Tanganyika na visiwa vya Zanzibar kufuatia uhuru wao kutoka Uingereza na mapinduzi ya Zanzibar.
Ndoa baina ya nchi hizo mbili katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikizidi kuzusha mijadala ambapo wakati wananchi wengi wa Tanzania bara wakionekana kuazimia kudumisha umoja wa kitaifa unaoletwa na muungano huo wenzao wa visiwani wamekuwa wakizidi kulalamika kwa kudhoofishwa kwa mamlaka yao ya dola.
Sokomoko hilo ni kitu kisichohitajika kabisa kwa serikali ya Rais Jakaya Kikwete ambaye ana shauku ya kuionyesha nchi hiyo kuwa ni nguzo ya utulivu na taifa kubwa la kiuchumi huko usoni kutokana na kuwa na sehemu kubwa ya ardhi ambayo bado kuendelezwa,neema ya rasimali za asili kama vile dhahabu,nikeli na Tanzanite, utalii unaonawiri na kugundulika kwa gesi asili nje ya fukwe hivi karibuni.
Aliyekuwa Profesa wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Abdul Sherrif hafikirii kuwa muungano huo ni imara zaidi kuliko ulivyokuwa hapo zamani kutokana na kwamba miaka mitatu iliopita watu walikuwa wakijadili mfumo mbadala wa muungano huo.
Rasimu ya katiba mpya
Ramani ya Tanzania.
Ramani ya Tanzania.
Hapo mwaka 2011 serikali ya Tanzania ilikubali kuutathmini muungano huo katika mfumo uliopo hivi sasa na kurasimu katiba mpya,ambapo tume maalum ilifanya ziara kwenye miji yenye wakaazi wengi, vituo vilioko mbali kwenye uwanda wa savana na kwenye fukwe za michanga meupe kujuwa maoni ya watu juu ya masuala mbali mbali yanayohusu maisha yao likiwemo hilo la muungano.
Mwezi uliopita rasimu mpya ya katiba iliwasilishwa kwenye Bunge la Katiba lenye wajumbe zaidi ya 600 ili kuijadili kabla ya kupigiwa kura ya maoni na wananchi.
Rasimu hiyo ya katiba inapendekeza kuundwa kwa shirikisho jipya litakalokuwa na serikali tatu tafauti: serikali zitakazojiamulia mambo yao wenyewe za Zanzibar na Tanganyika na serikali nyengine ndogo ya muungano kushughulikia masuala ya shirikisho kama vile ulinzi na mambo ya nje.
Pendekezo hilo liko kinyume kabisa na mundo wa sasa serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na ile yenye mamlaka yake ya visiwa vya Zanzibar muundo ambao serikali inataka kuendelea nao hata kama unashutumiwa na wananchi wa visiwani ambao wanasema hawana madaraka halisi mbele ya Tanzania bara ambayo ni kubwa na tajiri.
Mfumo mbadala wa muungano
Wanachama na wafuasi wa chama tawala Tanzania CCM.
Wanachama na wafuasi wa chama tawala Tanzania CCM.
Sehemu kubwa sana ya wananchi wa Zanzibar ni Waislamu na kuna mchanganyiko wa Waarabu, Wahindi na Waafrika.
Profesa Sherrif ambaye ni mjumbe wa bunge la katiba na mfuasi wa mageuzi anasema iwapo kutapatikana mfumo mbadala muungano huo yumkini ukazidi kuimarika.
Anasema "Lakini iwapo serikali itafanikiwa katika kuizuwiya na kuibadili,yumkini watu wakapiga kura ya kuipinga katiba hiyo na iwapo hilo litatokea itakuwa hatari sana.".
Profesa huyo anafananisha na hatari ya machafuko ya kisiasa ya umwagaji damu kama yale yaliyotokea katika nchi jirani ya Kenya hapo mwaka 2007.
Mdahalo waanza vibaya
Lakini mdahalo wa kuufanyia mageuzi muungano uliingia kwenye matatizo mara tu baada ya kuanza.Kauli mbaya za kukashifu viongozi na nyengine za kibaguzi ambao ulikuwa ukipigwa vita kwa nguvu zote na mmojawapo wa waasisi wa muungano huo na aliyekuwa baba wa taifa hilo Mwalimu Julius Nyerere na kuuita kuwa ni "dhambi" zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara kwenye mijadala ya bunge hilo huko Dodoma.

Jengo mashuhuri viswani Zanzibar la Beit- al -Ajaib.
Jengo mashuhuri viswani Zanzibar la Beit- al -Ajaib.
Mapema mwezi huu karibu wajumbe 200 wa bunge la katiba wengi wao wakitoka kwenye vyama vya upinzani na wawakilishi wengi wa Zanzibar walijitowa kwenye vikao vya bunge hilo kupinga kuburuzwa na chama tawala cha mapinduzi CCM ambacho kinadhibiti takriban theluthi mbili ya bunge hilo.
Sherrif anasema thelutji moja ya wajumbe wa bunge hilo wamelisusia bunge hilo akiwemo yeye mwenye na iwapo hawatorudi kwenye bunge hilo hakuna katiba itakayoweza kupitishwa kwa sasa.
Amesema "Iwapo muungano huo utaendelea kuwepo kwa miaka mengine hamsini kutategemea iwapo tutaweza kupata mfumo unaofaa ambapo pande zote mbili zinaweza kuishi na kwa ajili hiyo inabidi tusubiri."
Hata hivyo Rais Kiwete wa Tanzania amesema kwamba mfumo wa serikali tatu utakuwa na gharama kubwa mno na huenda hata ukavunja kabisa muungano wao wenyewe.
Uelekeo wa muungano bado haujulikani
Muasisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwl.Julius Nyerere.
Muasisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwl.Julius Nyerere.
Kutokana na kujitowa kwao huko bunge hilo halina tena wawakilishi wa kutosha kutoka Zanzibar kuichambuwa kisheria rasimu hiyo ya katiba kwa mujibu wa Bernadetta Killian profesa wa taaluma ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na pia ni mjumbe mwengine wa bunge hilo.
Amesema iwapo chama tawala kitashinikiza kupitishwa kwa rasimu bila ya kuhusishwa kwa upinzani mchakato huo utakuwa umekosa uhalali kwa hiyo hakuna uhakika kwa uelekeo wa muungano huo kwa sasa.
Wananchi wa Zanzibar katu hawakuwahi kushauriwa iwapo walikuwa wakitaka kujiunga na muungano huo au la.Hatimae miaka hamsini baadae wamepata fursa hiyo.
Hii ni mara ya kwanza kumekuwepo na mjadala wa wazi kuhusu muungano huo nchini Tanzania.Mambo mengi yaliokuwa yamefanyika nyuma ya pazia au faraghani juu ya makubaliano ya muungano huo na kusainiwa na waasisi wake ambao wote ni marehemu aliyekuwa Rais wa Tanganyika na baadae Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume sasa yanajadiliwa hadharani.
Kumekuwepo na matatizo tokea kuasisiwa kwa muungano huo mwaka 1964 na mara kwa mara watu walikuwa wakitabiri kwamba utasambaratika lakini umendelea kudumu.
Wachambuzi wanaona kwamba iwapo wataweza kuondokana na sokomoko la sasa muungano huo utazidi kuwa imara kuliko ulivyokuwa kabla.
Share on Google Plus

About Dira Ya Maisha

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Chapisha Maoni