Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kutia saini amri kuu kuweka masharti kuhusu wahamiaji wanaoingia nchini humo.
Taarifa kutoka Marekani zinasema ataanza kwa hatua ya kuimarisha usalama katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico atakapozuru makao makuu ya wizara ya usalama wa ndani baadaye Jumatano.
Aidha, anatarajiwa pia kutoa tangazo la kuidhinisha sheria kali zaidi za kupata visa kwa wageni kutoka eneo la Mashariki ya Kati na Afrika ambayo yana Waislamu wengi.
Miongoni mwa nchi zitakazoathiriwa na agizo la Trump ni Syria, Yemen, na Iraq.
Bw Trump ameandika kwenye Twitter kwamba leo itakuwa siku muhimu sana kwa usalama wa taifa la Marekani.
Mwandishi wa BBC David Willis kutoka Washington anasema hatua hiyo huenda ikayaudhi mashirika ya kibinadamu na yale ya kutoa misaada ikizingatiwa mzozo unaoendelea kwa sasa kuhusu hali ya wakimbizi wa Syria.
Wakati wa kampeni yake ya urais, Donald Trump aliahidi kufanyia mageuzi suala la uhamiaji Marekani.
Aligusia ujenzi wa ukuta kati ya Mexico na Marekani kuzuia wahamiaji haramu na kuwapiga marufuku Waislamu kuingia katika taifa hilo kama sehemu ya vita dhidi ya ugaidi. Baadaye alibadili msimamo kidogo na kufafanua kwamba watakachofanyiwa Waislamu ni kufanyiwa ukaguzi mkali kabla ya kuruhusiwa kuingia Marekani.
0 comments:
Chapisha Maoni