.

.

CHUO CHA MIPANGO YA MAENDELEO YA VIJIJINI (IRDP) KIMEONGEZA IDADI YA UDAHILI WA WANAFUNZI KUTOKA 14,417 HADI 16,663.

 Na Deborah Lemmubi -Dodoma.

Chuo cha Mipango ya Maedeleo Vijijini (IRDP) katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 kimeongeza idadi ya udahili na usajili wa wanafunzi kutoka 14,417 mpaka kufikia wanafunzi 16,663 na kuendelea kufanya tafiti na kutoa huduma za ushauri na uelekezi kwa kufanya tafiti saba.

Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Mkuu wa Chuo hicho Prof Hozen Mayaya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti katika chuo hicho katika mwaka wa fedha 2022/23.



Prof.Mayaya ameongeza kuwa chuo hicho kinaendelea kupitia mitaala ya mafunzo ya muda mrefu na kuandaa mitaala ya kozi mpya na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kujenga miundombinu ya kufundishia.

Akiendelea kutaja vipaumbele ameeleza kuwa chuo kinaendelea kuajiri watumishi wapya, kulipa stahili mbalimbali, kupandisha vyeo watumishi waliokidhi vigezo pamoja na kuboresha huduma za ustawi na kuongeza uwezo wa kielimu na kiutendaji kwa watumishi 396.

Aidha ameeleza kuwa chuo hicho kimejipanga kufanya ukarabati mkubwa na mdogo wa nyumba 13 za watumishi, kulipa madeni ya watumishi na watoa huduma, kutekeleza shughuli ambazo hazikutekelezwa katika Mpango Mkakati wa mwaka 2016/17-2020/21 pamoja na uendelezaji wa maeneo ya Miyuji Kaskazini, Chigongwe na Kiseke.

Kuhusu utekelezaji wa majukumu ya chuo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 Prof Mayaya ameeleza kuwa hadi kufikia Juni 2022, jumla ya watumishi 351 walipata mafunzo ya muda mfupi na watumishi 50 wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu ndani na nje ya nchi.

Amesema kuwa Jumla ya Shilingi bilioni 9 zimetumika kugharamia utekelezaji wa miradi ya uendelezaji na utunzaji wa miundombinu ya chuo ambapo Shilingi bilioni 5 zimetumika katika ujenzi wa kumbi Tatu za mihadhara na mabweni mawili ya wanafunzi wa kike.

Pia amesema kuwa kati ya Sh.bilioni 9, Shilingi bilioni 4 ambazo ni mapato ya ndani zimetumika kutekeleza miradi katika Kituo cha Mafunzo kilichopo Mwanza ikiwemo ujenzi wa mgahawa, jengo la utawala, maktaba na kununua ardhi kwa ajili ya upanuzi wa chuo.



Sambamba na hilo ameeleza kuwa Katika mwaka wa masomo 2021/22, chuo kimeendesha program za muda mrefu 31.

"Mpaka kufikia Juni 2022, washiriki 31 wa nje wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi.

"Kwa mwaka 2021/22, chuo kimesajili jumla ya wanafunzi 14,461. Aidha, jumla ya Wahitimu 8,200 wamehitimu mwezi Disemba, 2021.

"Katika mwaka wa fedha 2021/22, chuo kiliwezesha wahadhiri wake kufanya tafiti Saba zinazolenga kutatua matatizo ya kijamii, kiuchumi na kuchangia kuandaa sera na miongozo mbalimbali ya kitaifa.

"Chuo kinatekeleza mradi wa "Higher Education for Economic Transformation" ambao umetenga Shilingi bilioni 6.85 kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia, kujifunzia kwa kujenga jengo moja la taaluma, kuboresha mitaala na kuwajengea uwezo Wahadhiri".

Share on Google Plus

About Dira Ya Maisha

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Chapisha Maoni