.

.

SERIKALI YA TANZANIA KUSOMESHA WATAALAMU BINGWA ILI KUIMARISHA HUDUMA ZA KIBINGWA HAPA NCHINI

 Na Jackline Lendava-Dodoma.

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeongeza fedha za kusomesha wataalamu bingwa na bobezi kuanzia bilioni tatu hadi kufikia shilingi bilioni nane kwa mwaka wa fedha 2021/22 lengo likiwa ni kuimarisha huduma za kibingwa na bobezi nchini na  kuhakikisha kwamba idadi ya wagonjwa wanaopata rufaa za matibabu nje ya nchi inapungua .



Hayo yameelezwa Oktoba 28, 2022 jijini Dodoma na waziri wa afya Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa wataalamu wanaofadhiliwa kwenda kusoma nje na ndani ya nchi watafadhiliwa kwa utaratibu wa set kwa kila idara ya afya nchini.


"Ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na bobezi nchini kuanzia mwaka huu wa fedha, Wizara imeanzisha mkakati mpya wa kutoa ufadhili kwa watumishi wa Sekta ya Afya kwa utaratibu wa set. Kupitia utaratibu huu, utahusisha kusomesha timu za wataalamu wanaohitajika kwa ajili ya kukamilisha utoaji huduma za kibingwa na bobezi. Utaratibu huu umeanzishwa ili kuhakikisha huduma za kibingwa zinazotolewa zinakuwa na wataalamu wote wanaohitajika ili huduma husika iweze kutolewa kwa ukamilifu." Waziri Ummy



Sambamba na hilo waziri Ummy amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia Mpango wa kufadhili watumishi wa Afya katika fani za ubingwa na ubobezi, Wizara itatoa ufadhili wa mafunzo ya set yaliyowasilishwa na Taasisi mbalimbali katika maeneo ya kibobezi na kibingwa kupitia mpango wa set ambapo jumla ya watumishi 139 wamechaguliwa kupata ufadhili wa masomo na kati ya hao 136 watasomeshwa nje ya nchi na 3 ndani ya nchi na ili kumuenzi Mhe. Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuhakikisha ukamilifu wa huduma za kibingwa na bobezi Mpango huu umepewa jina la Mpango wa Samia wa kuongeza wataalamu bingwa na bobezi wa afya nchini (Samia Health Super Specialization Program in Tanzania). 



Hadi kufikia Disemba 2021, mahitaji ya wataalamu bingwa katika Hospitali zinazotoa huduma za kibingwa na kibobezi nchini yalikuwa 1,782 wakati huo Serikali ilikuwa imeshawasomesha wataalamu 992 wa fani mbalimbali za kibingwa na kibobezi huku hatua hiyo ikiwezesha uboreshaji wa huduma za afya za kibingwa na bobezi katika hospitali mbalimbali nchini hali ambayo imechangia kuimarika kwa huduma za matibabu nchini. 


"Hospitali zitakazonufaika kupitia na Mpango huu ni pamoja n hospitali ya Taifa Muhimbili kwa Upandikizaji figo ,upandikizaji uroto (Bone Marrow Transplant), Upandikizaji wa vifaa vya kusikia (Cochlear Implant) na upasuaji bobezi wa kinywa na uso. Hospitali ya Mloganzila kwa ubobezi katika  huduma za tiba za mfumo wa upumuaji na ubobezi katika huduma za wagonjwa wa kiharusi. Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ubobezi katika huduma za figo, ubobezi katika hduma za Saratani na Upandikizaji uroto. Taasisi ya Mifupa Muhimbili Kwa upasuaji wa mishipa ya damu kwenye ubongo na uti wa mgongo na Mazoezi tiba katika maradhi yanayotokana na ajali. Hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC kwa Matibabu ya kibobezi katika afya ya Ngozi, Huduma za Utengamao na huduma za mfumo wa Mkojo. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa huduma za kibingwa za matibabu ya Saratani. Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa ubobezi katika upasuaji wa Saratani na ubobezi katika tiba mionzi tiba na nyuklia (Radiotherapy & Nuclear Medicine)." Waziri Ummy 



Pia waziri Ummy amesema kuwa ufadhili huu, ni kwa ajili ya malipo ya ada kwa asilimia mia moja ya chuo husika na posho ya utafiti kwa waliopata ufadhili kwa vyuo vya ndani ya nchi na watakaofadhiliwa nje ya nchi watalipiwa ada kwa asilimia mia moja, posho ya utafiti, nauli pamoja na posho ya kujikimu wakiwa masomoni. 


"Pamoja na ufadhili kwa watumishi 457, jumla ya watumishi 524 wanaendelea na masomo katika fani mbalimbali za kibingwa na bobezi, hivyo kupelekea idadi ya wataalamu bingwa wanaofadhiliwa na Serikali kuwa 981. Jitihada hizi za Serikali zitaongeza idadi ya wataalamu bingwa na bobezi wanaohitimu kila mwaka ikilinganishwa na watumishi 259 waliohitimu mafunzo hayo kwa mwaka 2021/22. Majina ya wote waliochaguliwa kupata ufadhili kwa mwaka 2022/23 kwa mchanganuo nilioutaja hapo juu yatapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Afya (www.moh.go.tz)." Waziri Ummy

Share on Google Plus

About Dira Ya Maisha

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Chapisha Maoni