Na Mwaandishi Wetu-Arumeru.
Watendaji 26 wa Kata za Halmashauri ya Meru, Wilayani Arumeru wasaini mkataba wa Lishi ikiwa ni juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan za kupinga na kuzuia utapiamlo kwenye jamii ikizingatiwa lishe ni msingi wa afya ya binadamu, maendeleo ya jamii na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango wakati wa ufunguzi kikao cha Watendaji cha kusaini mikataba ya lishe, ameelekeza agenda ya lishe kuwa ya kudumu kwenye mikutano kuanzia ngazi za vijiji na Kata ambapo amewataka watendaji hao kushirikiana na watalamu wa lishe kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano sambamba na kuhamasisha jamii kutumia makundi matano ya vyakula.
Mhe.Ruyango amesema Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo imetoa zaidi ya milioni 120 za afua za lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 katika Halmashauri ya Meru hivyo ametoa wito kwa viongozi wa ngazi zote kuunga mkono jitihada hizo za Serikali kwa kusimamia vyema maswala ya lishe kwenye maeneo yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl.Zainabu Makwinya ambaye ameingia Mkataba na watendaji wa Kata 26 za Halmashauri hiyo ametoa wito kwa watendaji na jamii kushiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wa mkataba huo wa lishe unaolenga kuwa na jamii bora ambapo amemshukuru Mhe.Rais kuwa mstari wa mbele latika kuimarisha suala la lishe.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti watendaji wa Kata wameahidi kusimamia vyema mikataba hiyo ambapo wameishukuru Serikali kwani mbali na mikataba hiyo imewapa vitendea kazi yaani usafiri utakao wawezesha kuifikia jamii"tunaishukuru Serikali kutupa pikipiki 3 kwa ajili ya ufuatiliaji wa masula ya lishe"ameshukuru Elibariki Molel Afisa Mtendaji Kata ya Usa River.
Zoezi hilo la utiaji saini mikataba ya lishe limefanyika katika ukumbi wa Halmashauri kushuhudiwa na wakuu wa Idara na Vitengo, Kamati ya uendeshaji huduma za afya ngazi ya Wilaya na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Arumeru.
0 comments:
Chapisha Maoni