Na Onesmo Elia Mbise,
Arusha
eliaonesmo@gmail.com
Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kwa kushirikiana na (TANAPA) imeanza zoezi la kuyaachia makundi manne ya Mbwa mwitu wapatao ishirini (20) katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa lengo la kuendeleza mfumo ikolojia kwa ustawi wa uhifadhi na kukuza utalii.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo ambalo limefanyika katika eneo la Makoma Serengeti, Dkt.Emmanuel Masenga ambaye ni Mtafiti Mkuu TAWIRI na Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori Serengeti amesema zoezi la kurejesha Mbwa mwitu katika hifadhi ya Taifa Serengeti ni endelevu kutokana na umuhimu wa wanyamapori hao katika mfumo wa Ikolojia.
Dkt.Masenga amesema wataendelea kuwafuatilia mbwa hao kupitia visukuma mawimbi baada ya kuwaachia ikiwa ni kuhakisha azma ya Serikali ya kuwarejesha kwa wingi mbwa mwitu ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti inatimia kwa ajili ya kutunza bioanuwai hii isitoweke.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Moronda B. Moronda kutoka TANAPA amesema zoezi hilo kuwarejesha mbwa mwitu ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti lina manufaa katika uhifadhi kwani kuongezeka kwa Mbwa mwitu ni zao zuri la utalii, na watalii wataweza kufurahia na kushuhudia namna wanyamapori hawa wanavyowinda tofauti na ilivyozoeleka kuwaona Simba.
Aidha, Maronda ametoa wito kwa wananchi wanaopakana na hifadhi kutoa taarifa pale wanapowaona Mbwa mwitu katika maeneo yao na kutokuwaua kutokana na uwepo wa idadi ndogo ndani ya Hifadhi.
0 comments:
Chapisha Maoni