NA KHATIB SULEIMAN, ZANZIBAR
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wananchi wanaoishi katika kata 19, zitakazofanya uchaguzi mdogo wa madiwani kwa upande Tanzania Bara na ubunge katika Jimbo la Dimani Zanzibar leo, wajitokeze kwa wingi kupiga kura kuwachagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mwenyekiti wa NEC Jaji Semistocles Kaijage
Akizungumza na vyombo vya habari mjini Zanzibar jana, Mwenyekiti wa NEC Jaji Semistocles Kaijage alisema kuwa maandalizi ya uchaguzi huo, yamekamilika.
Kwamba wananchi wenye sifa za kupiga kura katika uchaguzi huo, wajitokeze kutimiza wajibu wao wa kikatiba.
Kaijage aliwapongeza wananchi wanaoishi katika Jimbo la Dimani, na wale wa Kata 19 za Tanzania Bara, zitakazofanya uchaguzi mdogo leo kwa utulivu, waliouonesha wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi huo.
Alieleza kuwa licha ya kuwepo kwa dosari za hapa na pale zilizojitokeza, zikiwemo za ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi kwa baadhi ya vyama na wagombea wao, NEC ilichukua hatua za kukemea vitendo hivyo ili kuwezesha kampeni za uchaguzi kufanyika kwa usalama na amani.
“Licha ya kwamba kutakuwa na ulinzi wa kutosha katika vituo vya kupigia kura, ni matumaini ya Tume kuwa hali ya amani na utulivu ambayo imekuwepo hadi sasa na kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita itaendelea kudumishwa ili kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa utulivu, amani na ustawi wa Taifa letu,” alisema Jaji Kaijage.
Alieleza kuwa katika uchaguzi huo, jumla ya wapiga kura 9,280 wa Jimbo la Dimani Zanzibar wanatarajiwa kupiga kura ili kumchagua mbunge, atakayewaongoza kwa kipindi cha miaka mitatu kupitia vituo 29 vya kupigia kura katika Jimbo hilo.
Kwa upande wa uchaguzi mdogo wa madiwani katika Kata 20 za Tanzania Bara, wapiga Kura 134,705 walioandikishw,a wanatarajia kupiga kura katika vituo 359 ambavyo vilitumika katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015
0 comments:
Chapisha Maoni