.

.

UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NA KUJIELEZA UNAHITAJI SHERIA RAFIKI

Mwandishi wetu

Uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza ni moja ya mambo muhimu katika taifa lolote la kidemokrasia.

Kutokana na umuhimu huo katika mataifa mengi kumekuwepo na maboresho ya mara kwa mara ya sheria ili kwendana na wakati.

Hata hivyo baadhi ya maboresho badala ya kuboresha uhuru huo yamekuwa yakiminya uhuru.



Hivyo kwa hapa nchini ndioMaana kuna mijadala ,mafunzo na uchechemuzi  juu ya sheria  kadhaa ikiwepo zinazolenga uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.

Taasisi ya vyombo vya habari ya Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania(MISA-Tan) Jukwaa la wahariri(TEF) baraza la habari(MCT) Chama cha  wafanyakazi waandishi wa habari (JOWUTA) wamekuwa wakitoa elimu na mapendekezo kadhaa ya uboreshwaji sheria za habari na uhuru wa kujieleza nchini.

Pia kuna kazi ya utoaji wa elimu na kufanya uchechemuzi juu ya sheria za habari unaofanywa na Chama cha waandishi wa jamii za pembezoni(MAIPAC) Umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini(UTPC) chama cha waandishi wa habari wanawake(TAMWA) na chama cha waandishi kupambana na madawa ya kulevya(OJADACT) wadau  wa habari wakiwepo mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu(THRDC) na kituo cha sheria na haki za binaadamu(LHRC) na   mapendekezo kadhaa kuboresha sheria za habari yametolewa.

MISA imekuwa na mradi wa kuelimisha juu ya sheria za habari uzuri na mapungufu yake na wamefanyakazi kubwa sana karibu nchi nzima.

Mchakato huu haupo kwa kubahatisha bali ni utekelezwaji wa Azimio la umoja wa mataifa la haki za binaadamu kifungu cha 19  ambacho kinaeleza kila mmoja ana haki ya uhuru wa kutoa na kueleza maoni yake; haki hii inahusu pia uhuru wa kushikilia maoni yake bila kuingiliwa kati na uhuru wa kutafuta na kutoa habari na maoni kwa njia  yoyote bila kujali mipaka.

Kifungu hiki kinafanana kabisa  na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18.(1)  ambacho  kinasomeka Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati..

Katika miaka ya karibuni hapa nchini, kumetungwa  baadhi ya  sheria ambazo zinavifungu   zinavyokinzana na Azimio la haki za binaadamu la umoja wa mataifa lakini pia Katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania.vifungu ambavyo vinaathiri utendaji wa makundi kadhaa katika jamii wakiwepo wanahabari.

Baadhi ya vifungu ambavyo vinahitaji marekebisho, vipo katika sheria ya Sheria ya Huduma za Habari  ya mwaka 2016, Sheria ya makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Mawasiliano ya kielektroniki na Posta 2010, Kanuni za Mwasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Habari za Mtandaoni )2018 na Sheria ya kupata habari, 2016

Hata hivyo, tangu kupitishwa sheria hizo, imebainika wazi kuna baadhi ya maeneo zinatumika vibaya kuminya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni .



Sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016 ina mapungufu kadhaa ikiwepo Kifungu cha 50 cha sheria hii  kinaeleza makosa na adhabu kwa kuchapisha habari kwa makusudi, uzembe , ya kutungwa na ya uongo, yenye nia ovu au ya kutungwa na ya uongo, au taarifa iliyokatazwa inayoweza kuhatarisha maslahi ya jamii, na hadhi, haki au uhuru wa watu wengine.

Makosa haya ya uchochezi yamefanywa ya kijinai na adhamu yake  ni kutozwa faini kuanzia milioni tano na usiyozidi millioni 10 au kifungo kuanzia miaka mitatu na kisichozidi miaka mitano au vyote pamoja.

Lakini pia muundo ya baraza huru za habari, utaratibu wa kutoa leseni kwa vyombo vya habari na leseni ya kufanyakazi wanahabari kunachangamoto kadhaa ambazo zinapaswa kuboreshwa ili kurejesha uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari.

Wadau wa habari  wamekuwa na hoja kuondoa makosa haya ya kitaaluma kuwa ya kijinai kwani ni sawa na makosa ya wanataaluma wengine wanapofanya wakiwa kazini na wamekuwa hawashitakiwi kwa kufanya jinai.

Katika Sheria ya kupata habari, 2016  inaorodhesha makosa anuai, yakiwemo kupotosha taarifa ambayo  adhabu ya kifungu cha kati ya miaka miwili hadi mitano gerezani kuna mapungufu kadhaa katika sheria hii.

Sheria ya Mawasiliano ya kielektroniki na Posta 2010 Masuala ya maudhui Kifungu cha 103-4 kinaeleza kuhusu kanuni za maadili zenye nguvu ya kisheria, na zinapiga marufuku kutangaza maudhui ya uongo, yenye matusi, yenye vitisho, na yanayokiuka maadili ya jamii au yanayokwaza kwa ujumlaHowungu cha 107 cha kanuni ya maudhui ya mtandao  kinaeleza kuhusu udhibiti wa maudhui huru, yanayoendana na yanayoakisi uhalisia wa Tanzania, na kinazuia urushaji wa vipindi vyenye maudhui yasiyoendana au kuwa na umuhimu kwa maendeleo na mazingira ya kijamii nchini Tanzania. 

Kifungu hicho pia kinaeleza kiwango ambacho maudhui huru, na yanayoendana na kuakisi mazingira ya Tanzania yatajumuishwa; vilevile kinaeleza muda wa siku na wiki ambapo maudhui hayo yatarushwa hewani. 

Sheria haikatazi kurusha matangazo yenye maudhui ya kisiasa. Hata hivyo, Waziri anaweza kudhibiti matangazo hayo kwa namna inayoendana na malengo, maelekezo na kanuni, haki za msingi na wajibu kama ilivyoainishwa kwenye Katiba

 Athari ya kanuni hizi,  Mamlaka ya Mawasiliano imepewa madaraka makubwa mno katika kudhibiti maudhui kwa kutumia lugha butu na maneno kama vile “ya matusi”, inayokiuka maadili”, “ya vitisho”, na “inayokwaza” yasiyofafanua masuala muhimu kwa ufasaha. 

Itakuwa vigumu kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari kufahamu au kutarajia aina ya maudhui yanayokwenda kinyume na Sheria hii, Kwa kufanya hivyo, Serikali inakuwa na nguvu isiyohojika kuweza kupiga marufuku maudhui yasiyoipendeza wakati wowote inapotaka kufanya hivyo.

Lakini pia kanuni hizi, zimempa Waziri mamlaka makubwa sana ya kutumia busara zake kuelekeza namna namna ambavyo kutangaza vipindi vya maudhui ya kisiasa, hali inayoathiri uhuru wa sera huru ya uhariri kwenye vyombo vya habari.  

 Sheria ya Makosa ya Mtandao pia  Sheria hii inahusu makosa yanayohusiana na mifumo ya kompyuta na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki na unaohusiana na hayo. 

Katika sheria hii, baadhi ya vifungu vina athari zake kwa tasnia ya habari ni pamoja na Makosa na Adhabu , Vifungu vya 4-29 vinaeleza kuhusu makosa na adhabu kuhusiana na mifumo ya kompyuta.

katika sheria hii  Kifungu cha 20 kinaainisha makosa kwa kusambaza, au kurusha au kusambaza tena taarifa zinazotumwa bila ridhaa, au kughushi taarifa za utambulisho na kuzituma bila ridhaa, yaani taarifa au data za kielektroniki ambazo hajaikuombwa na mpokeaji.

Hata hivyo sheria hii inaathari, baadhi ya Vifungu vya sheria vinavyoainisha au kufafanua makosa vinaweza kutumika kuadhibu waandishi wa habari, wafichua uhalifu, na wafuatiliaji wa utendaji wa vyombo au taasisi mbalimbali,Vipengele hivi vinaweka  adhabu hata kama hakukuwa na nia ya kutenda jinai au madhara makubwa kwa mwathirika.

Hivyo, matumizi halali na yasiyokuwa na nia ovu ya data au taarifa kwenye mfumo wa kompyuta yamejinaishwa, waandishi wa habari, ambao kazi zao zinahusisha na  kubadilishana taarifa  wanaweza kukutwa na makosa kwa vitendo walivyofanya bila ya kuwa na nia ovu pindi wanapopokea au kusambaza taarifa  wakiamini kwamba wanaruhusiwa kufanya hivyo bila ya kufahamu muktadha wa namna taarifa hizo zilivyosambazwa au kupatikana.

Hivyo kwa uchache haya ni baadhi tu ya mapungufu katika sheria ambazo kinaathiri uhuru wa vyombo vya habari, kufanyakazi kwa weledi lakini pia vinaathiri uhuru wa utoaji maoni  na vinapaswa kuboreshwa kwendana  na matakwa ya Katiba na Azimio la umoja wa mataiiiifa za haki za binaadamu na sheria mbali mbali za kimataifa.

Tanzania sio kisiwa  hivyo ni muhimu kuwa na sheria rafiki ambazo zinalinda na kutetea uhuru wa vyombo vya habari na  kujieleza kama ambavyo Katiba ya nchi inaeleza lakini pia kama tulivyoridhia mikataba na matamko kadhaa ya umoja wa mataifa.

 Mwandishi wetu anapatikana namba Kwa Namba  za simu 0759034780

Share on Google Plus

About Dira Ya Maisha

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Chapisha Maoni